Pokeeni salamu nyingi kutoka kwangu (Mch. Dktr. B. Mtokambali - Askofu Mkuu) na viongozi wenzangu wa kamati kuu ya utendaji. Nimefarijika sana kwa taarifa nilizopata kutoka kila kona ya nchi yetu ya Tanzania jinsi washirika wetu walivyoshiriki kwenye juma la maombi maalum kwa ajili ya janga hili la virusi vya Corona (COVID-19). Mungu awabariki.
Hata hivyo kwa kuwa janga hili bado linaendelea, hatutakoma kuomba kama vile Biblia inavyotuelekeza kwenye Luka 18:1. Hivyo basi, naomba nitoe maelekezo yafuatayo:-
- Tunaitenga siku ya Ijumaa kuwa siku ya kufunga na kuomba kwa kanisa zima la TAG. Hivyo basi, tunawaita wa-TAG wote nchi nzima kuendelea kufunga na kuomba na kukutana kila Ijumaa bila kukoma wala kukata tamaa.
- Nahimiza kuwa, kwenye maombi yetu ya Kanda yaliyopo kwenye kalenda yetu, agenda kubwa iwe ni kumsihi Mungu juu ya janga hili la virusi vya Corona hadi ufumbuzi upatikane, kwani Mungu wetu hajawahi kushindwa na kitu kamwe.
- Nashauri kila kanisa liimarishe ibada za nyumba kwa nyumba kama kwenye kanisa ya Matendo ya Mitume (Mdo 2:16). Hii itatusaidia kuendelea kuwa na ibada hata kama itatokea Serikali kusitisha ibada za makanisani kama nchi nyingi duniani zilivyositisha (Mithali 27:12).
- Naelekeza kila kanisa la TAG na kila mshirika wa TAG azingatie maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika (yaani Serikali na Shirika la Afya Duniani - WHO) ili kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo (Rumi 13:1-2, 2 Tim 1:7, Mithali 18:10).
Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinyenyekesha na kunitafuta uso, nitawasikia na kuiponya nchi yao.
2 Mambo ya Nyakati 7:14
Nawatakia baraka za Bwana
Add Comment