Misingi 16 ya Imani yetu

Imani yetu umejengwa katika misingi 16

Tunaamini kwa dhati kuwa Biblia ndio Mwongozo wa imani yetu na matendo katika maisha yetu ya Kikristo. Tamko hili ndilo msingi wa ushirika wetu (1Kor.1:10; Mdo.2:42). Ukiri wa Imani yetu umejengwa katika misingi kumi na sita (16) ifuatayo:

Tunaamini kwamba Maandiko yote ya Agano la Kale na yale ya Agano Jipya yamevuviwa kihalisi na Mungu na ni Ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu, ni mamlaka ya mwisho ya imani (2Tim.3:15-17; 1The.2:13; 2Pet. 1:2)

Tunaamini kwamba Mungu mmoja tu aliye hai na wa kweli amekwisha kujifunua mwenyewe kama “MIMI NIKO” wa milele, muumbaji wa mbingu na nchi na Mkombozi wa Ulimwengu na Wanadamu. Yeye pia amejifunua zaidi kama mwenye kufuata mwenendo na ushirikiano na uhusiano katika Baba, Mwana na Roho Mtakatifu (Kumb. 6:4; Isa.43:10,11; Mat.28:19; Lk.3:22).

Tunaamini kwamba Bwana Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu na ana sifa zote za Uungu (Yoh.1:1; 8:58; Isa.9:6; 1Yoh.5:20). Maandiko yanatangaza:
(i) Kuzaliwa kwake na bikira (Mt.1:23; Lk.1:31:35).
(ii) Maisha yake yasiyo na dhambi (Ebr.7:26; 1Pet.2:22).
(iii) Miujiza yake (Mdo. 2:22, 10:38).
(iv) Kazi yake ya malipizi juu ya msalaba (1Kor.15:3, 2Kor.5:21).
(v) Ufufuo wake kimwili kutoka katika wafu (Mt.28:6; Lk.24:39, 1Kor.15:4).
(vi) Kutukuzwa kwake kwenye mkono wa kuume wa Mungu (Mdo.1:9; 11; 2:33; Fil.2:9-11; Ebr.1:3).

Tunaamini kwamba mwanadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu akiwa mzuri na mwema, maana Mungu alisema: “Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu”. Hata hivyo mwanadamu kwa uasi wa hiari yake mwenyewe alianguka na kwa njia hiyo akajiletea mauti siyo ya kimwili tu, bali pia mauti ya kiroho ambayo ni kutengwa na Mungu (Mwa.1:26, 27; 2:17; 3:6; Rum. 5:12-19).

Tunaamini kwamba tumaini la pekee la mwanadamu la ukombozi ni kwa njia ya damu ya Yesu Kristo, mwana wa Mungu iliyomwagika.
(i) Masharti ya Wokovu:
Tunaamini kwamba wokovu hupatikana kwa njia ya toba mbele za Mungu na imani kwa Bwana Yesu Kristo. Kwa kuoshwa kwa kufanywa upya na kuzaliwa mara ya pili kwa njia ya Roho Mtakatifu, kuhesabiwa haki kwa neema kwa njia ya imani, mwanadamu hufanyika mrithi wa Mungu kulingana na tumaini la uzima wa milele (Lk.24:47; Yoh.3:3; Rum.10:13-15; Efe. 2:8; Tito 2:11; 3:5-17).
(ii) Ushahidi wa Wokovu:
Tunaamini kwamba ushahidi wa wokovu ulio wa ndani ni ushuhuda wa moja kwa moja wa Roho Mtakatifu (Rum. 8:16). Ushahidi wa nje kwa watu wote ni ya haki na utakatifu wa kweli (Efe. 4:24; Tito 2:12).

(i) Ubatizo katika Maji Mengi:
Tunaamini juu ya agizo la ubatizo wa kuzamisha linatolewa katika Maandiko. Wote wanaotubu na kumwamini Kristo kama Mwokozi na Bwana wanaweza kubatizwa. Kwa njia hiyo, wanautangazia ulimwengu kwamba wao wamekufa pamoja na Kristo na pia kwamba wao wamefufuliwa pamoja naye ili kuenenda katika upya wa uzima (Mt.28:19, Mk.16:6; Mdo.10:47, 48; Rum. 6:4).
(ii) Ushirika Mtakatifu:
Tunaamini juu ya meza ya Bwana ambayo ina mkate na matunda ya mzabibu ni mfano wa kuelezea ushirika wetu wa asili ya ki-Mungu na Bwana wetu Yesu Kristo (2 Pet.1:4). Ni kumbukumbu ya mateso yake na kifo chake (1Kor.11:26) na ni sharti kwa waamini wote hata ajapo.

Tunaamini kwamba waamini wote wanatakiwa na wanayo haki ya kutafuta ahadi ya baba, yaani ubatizo wa Roho Mtakatifu, kulingana na agizo la Bwana wetu Yesu Kristo. Huu ulikuwa ni ujuzi wa kawaida kwa wote waliokuwemo katika kanisa la mwanzo la Kikristo. Pamoja na huo ubatizo huja uwezo kutoka kule juu kwa ajili ya maisha ya utumishi, na kutolewa kwa karama pamoja na matumizi yake katika huduma (Lk.24:49; Mdo.1:4; 8; 1Kor.12:1-31). Ujuzi huu ni tofauti kabisa ingawa unalingana na ujuzi wa kuzaliwa upya (Mdo.8:12-17; 10:44-46;11:14-16; 15:7-9).

Pamoja na ujuzi huo wa ubatizo katika Roho Mtakatifu kunakuja ujuzi mwingine kama kujazwa mpaka kufurika kwa Roho Mtakatifu (Mdo.2:43, Ebr.12:28), kujitoa kwa hali ya juu kwa ajili ya Mungu na kujiweka wakfu kwa ajili ya kazi yake (Mdo.2:42), pamoja na upendo wenye vitendo zaidi kwa Kristo na kwa Neno lake na kwa wanaopotea (Mk.16:20).

Tunaamini kwamba ubatizo wa waamini katika Roho Mtakatifu unashuhudiwa kwa ishara ya nje iliyo ya kimwili ya kunena kwa lugha nyingine kama Roho wa Mungu anavyowajalia hao kutamka (Mdo.2:4). Huku kusema kwa lugha ni sawa sawa na ile karama ya aina za lugha (1Kor.12:4-10,28) ingawa ni tofauti katika makusudi na matumizi.

Tunaamini kwamba utakaso ni tendo la kutengwa na kile kilicho kiovu na kujiweka wakfu kwa ajili ya Mungu (Rum. 12:1,2; 1Thes. 5:23; Ebr.13:12). Maandiko yanatufundisha juu ya maisha ya utakatifu ambao pasipo huo hakuna mtu atakayemwona Mungu (Ebr. 12:12-14). Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu sisi tunao uwezo wa kutii amri ile: “Iweni watakatifu kama mimi nami nilivyo Mtakatifu” (1Pet. 1:15,16). Utakaso huwa halisi katika mwamini kwa kugundua na kufahamu utambulisho wake na Kristo katika kifo chake na kufufuka kwake, na kwa imani akijihesabia kila mara kwamba yumo katika muungano huo, na kwa kutoa kila kiungo kila mara kwa utawala wa Roho Mtakatifu (Rum. 6:1-11;13; 8:12;13; Gal.2:20; Filp. 2:12; 13; 1Pet. 1:15).

Tunaamini kwamba kanisa ni mwili wa Kristo, makao ya Mungu kwa njia ya Roho, lenye vyeo vya ki-Mungu kwa ajili ya utimizo wa kazi yake kuu. Kila mwamini aliyezaliwa kwa Roho ni sehemu muhimu ya kanisa ambalo ni kusanyiko la wazaliwa wa kwanza walioandikwa Mbinguni (Efe.1:22;23; 2:22; Ebr.12:23).

Tunaamini kwamba huduma ya ki-Mungu pamoja na utumishi uliopangwa na maandiko umetolewa na Bwana wetu kwa makusudi matano:
(a) Kuushuhudia ulimwengu (Mk 16:15);
(b) Kujengwa kwa mwili wa Kristo (Efe.4:11-13);
(c) Kuabudu (Yh.4:23-24);
(d) Utumishi (1Kor.12; Rum.12);
(e) Ushirika (Mdo.2:42-46).

Tunaamini kwamba uponyaji wa kimungu ni sehemu muhimu ya Injili. Kufunguliwa kutoka magonjwa na vifungo mbalimbali ni haki ya kila anayeamini (Isa. 53:4; 5; Mt. 8:16;17; Yak. 5:14-16).

Tunaamini juu ya ufufuo wa wale ambao wamelala katika Kristo na kunyakuliwa kwao pamoja na wale walio hai waliosalia mpaka wakati wa kuja kwake Bwana ndilo tumaini lenye baraka na lililo kuu la Kanisa (1Thes.4:16, 17; Rum. 8:23; Tito 2:13; 1Kor.15:51, 52).

Tunaamini kuja kwa mara ya pili kwa Kristo ni pamoja na kunyakuliwa kwa Watakatifu ambalo ni tumaini lenye baraka, kukifuatiwa na kurudi kwa wazi kwa Kristo pamoja na Watakatifu wake kwa ajili ya kutawala hapa Ulimwenguni kwa muda wa miaka elfu moja (Zek. 14:5; Mt. 24:27;30; Ufu.1:7; 19;11-14; 20:1-6). Utawala huu wa miaka elfu moja utaleta wokovu kwa Israeli kama taifa (Eze. 37:21,22; Zef.3:19, Zab. 72:3-8; Mika 4:3,4).

Tunaamini kwamba kutakuwepo na hukumu ya mwisho ambayo humo wafu waovu watafufuliwa na kuhukumiwa sawa sawa na matendo yao. Yeyote, ambaye hatakutwa ameandikwa katika Kitabu cha Uzima, pamoja na Shetani na malaika zake, mnyama na nabii wa uongo, watatupwa katika adhabu ya milele katika ziwa liwakalo moto na kibiriti, ambayo ni mauti ya pili (Mt. 25:46; Mk.9:43-48; Ufu. 19:20;20:11-15; 21:8).

Kulingana na ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya ambamo haki yakaa ndani yake (2Pet.3:13; Ufu. 21 na 22).