Tunachokiamini

Katika Tanzania Assemblies of God tunaamini katika kweli za msingi kumi na sita (16)
 
1. Tunaamini kwamba: Maandiko yamevuviwa na Mungu
Maandiko yote yakijumuisha yale ya Agano la kale na Agano jipya, yamevuviwa na Mungu na ndio ufunuo wa Mungu kwa wanadamu – hayana makosa, yana mamlaka juu ya Imani na maisha (2 Timotheo 3:15-17; 1 Wathesalonike 2:13; 2 Petro 1:21).
 
2. Tunaamini kwamba: Kuna Mungu mmoja aliyedhihirishwa katika nafsi tatu
Mungu aliye wa pekee amejidhihirisha kuwa wa milele “MIMI NIKO”, Muumbaji wa Mbingu na Nchi na Mkombozi wa wanadamu. Amejifunua katika ushirika wa utatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu (Kumbukumbu la torati 6:4; Isaya 43:10-11; Mathayo 28:19)
 
3. Tunaamini juu ya: Uungu wa Bwana Yesu Kristo
Bwana Yesu Kristo ni Mwana wa Milele wa Mungu. Maandiko yanatamka:
.
(a) Kuzaliwa kwake na Bikira  (Mathayo 1:23; Luka 1:31,35) 
(b) Maisha yake yasiyo na dhambi (Waebrania 7:26; 1 Petro 2:22) 
(c) Miujiza yake (Matendo ya Mitume 2:22; 10:38) 
(d) Kazi yake ya ukombozi Msalabani (1 Wakorintho 15:3; 2 Wakorintho 5:21) 
(e) Kufufuka kwake kutoka kwa wafu (Mathayo 28:6; Luka 24:39; 1 Wakorintho 15:4) 
(f) His exaltation to the right hand of God (Matendo 1:9,11; 2:33; Wafilipi 2:9-11; Waebrania1:3) 
 
4. Tunaamini juu ya Anguko la Mwanadamu 
Mwanadamu aliumbwa katika hali ya ukamilifu maana Mungu alisema: “Na tumfanye mtu kwa mfano wetu na sura yetu.” Hata hivyo, kwa hiari yake mwanadamu alianguka (aliasi) na hivyo kupelekea siyo tu mauti ya mwili, bali ya kiroho pia, ambayo ni kutengwa na Mungu God (Mwanzo 1:26,27; 2:17; 3:6; Warumi:12-19). 
 
5. Tunaamini juu ya: Wokovu wa Mwanadamu 
Tumaini pekee la ukombozi kwa mwanadamu ni kwa njia ya Damu ya Yesu Kristo Mwana wa Mungu. 
.
  (a) Masharti ya Wokovu
Wokovu tunaupata kwa njia ya Toba kwa Mungu na kumwamini Yesu Kristo. Kwa kuoshwa na kuzaliwa upya kwa Roho Mtakatifu na kuhesabiwa haki kwa njia ya Imani kwa Bwana Yesu Kristo, mwanadamu anafanyika mrithi wa Mungu kwa kadiri ya tumaini la uzima wa milele (Luka 24:47; Yohana 3:3; Warumi 10:13-15; Waefeso 2:8; Tito 2:11; 3:5-7). 
.
  (b) Ushahidi wa wokovu 
Ushahidi wa ndani wa wokovu ni kazi ya Roho Mtakatifu (Warumi 8:16). Ushahidi wan je wa wokovu kwa watu wote ni maisha ya haki na utakatifu wa kweli (Waefeso 4:24; Tito 2:12).
 
6. Tunaamini juu ya: Maagizo ya Kanisa
.
   (a) Ubatizo wa maji
Agizo la ubatizo wa kuzamishwa katika maji mengi umeamriwa katika Maandiko. Wote wanaotubu na kumwamini Kristo kama Mwokozi na Bwana wanapaswa kubatizwa. Kwa njia hiyo wanatangaza kwa ulimwengu kwamba wamekufa pamoja na Kristo na kwamba wamefufuka  pamoja naye ili kuishi pamoja naye katika upya wa maisha.
(Mathayo 28:19; Marko 16:16; Matendo 10:47,48; Warumi 6:4). 
.
  (b) Meza ya Bwana (Ushirika Mtakatifu)
Meza ya Bwana ambayo inahusisha – mkate na matunda ya mzabibu ni alama ya ushirika wetu katika asili ya kimungu ya Bwana wetu Yesu Kristo (2 Petro 1:4);
Ukumbusho wa kuteswa kwake na mauti (1 Wakorintho 11:26); taraja la kurudi kwake  (1 Wakorintho 11:26); na kuwaunganisha waamini wote “hata ajapo!” 
 
7. Tunaamini juu ya: Ubatizo wa Roho Mtakatifu
Waamini wote wanatakiwa na wanayo haki ya kutafuta ahadi ya baba, yaani ubatizo wa Roho Mtakatifu na moto, kulingana na agizo la Bwana wetu Yesu Kristo. Huu ulikuwa ni ujuzi wa kawaida kwa wote waliokuwemo katika kanisa la mwanzo la Kikristo. Pamoja na huo ubatizo huja uwezo kutoka kule juu kwa ajili ya maisha ya utumishi, na kutolewa kwa karama pamoja na matumizi yake katika huduma
(Lk.24.24:49; Mdo.1:4;8; 1Kor.12:1-31).
Ujuzi huu ni tofauti kabisa ingawa unalingana na ujuzi wa kuzaliwa upya (Mdo.812-17,10:44-46;11:14-16;15:7-9). 
.
Pamoja na ujuzi huo wa ubatizo katika Roho Mtakatifu kunakuja ujuzi mwingine kama kujazwa mpaka kufurika kwa Roho Mtakatifu (Mdo.2:43, Ebr.12:28), kujitoa kwa hali ya juu kwa ajili ya Mungu na kujiweka wakfu kwa ajili ya kazi yake (Mdo.2:42), pamoja na upendo wenye vitendo zaidi kwa Kristo na kwa Neno lake na kwa wanaopotea(Mk.16:20).
 
8. Ushahidi wa Ubatizo katika Roho Mtakatifu: 
Ubatizo wa waamini katika Roho Mtakatifu unashuhudiwa kwa ishara ya nje iliyo ya kimwili ya kunena kwa lugha nyingine kama Roho wa Mungu anavyowajalia hao kutamka (Mdo.2:4). Huku kusema kwa lugha ni sawa sawa na ile karama ya aina za lugha (1Kor.12:4-10,28) ingawa ni tofauti katika makusudi na matumizi.
 
9. Utakaso: 
Ni tendo la kutengwa na kile kilicho kiovu na kujiweka wakfu kwa ajili ya Mungu (Rum.12:1,2; 1Thes. 5:23; Ebr.13:12). Maandiko yanatufundisha juu  ya maisha ya utakatifu ambao pasipo huo hakuna mtu atakayemwona Mungu
(Ebr. 12:12-14).
 
Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu sisi tunao uwezo wa kutii amri ile: “Iweni watakatifu kama mimi nami nilivyo Mtakatifu” (1Pet. 1:15,16).
Utakaso huwa halisi katika mwamini kwa kugundua na kufahamu utambulisho wake na  Kristo katika kifo chake na kufufuka kwake, na kwa imani akijihesabia kila mara kwamba yumo katika muungano huo, na kwa kutoa kila kiungo kila mara kwa utawala wa Roho Mtakatifu (Rum. 6:1-11;13; 8:12;13; Gal.2:20; Filp. 2:12; 13; 1Pet. 1:15).
 
10. Kanisa: 
Kanisa ni mwili wa Kristo, makao ya Mungu kwa njia ya Roho, lenye vyeo vya ki-Mungu kwa ajili ya utimizo wa kazi yake kuu. Kila mwamini aliyezaliwa kwa Roho ni sehemu muhimu ya kanisa ambalo ni kusanyiko la wazaliwa wa kwanza walioandikwa Mbinguni (Efe.1:22;23; 2:22; Ebr.12:23).
 
11. Huduma: 
Huduma ya ki-Mungu pamoja na utumishi uliopangwa na  maandiko umetolewa na Bwana wetu kwa makusudi matano: 
(A) Kuushuhudia ulimwengu; 
(B) Kujengwa kwa mwili wa Kristo (Efe.4:11-13);
(C) Kuabudu (Yh.4:23-24); 
(D) Utumishi (1Kor.12;  Rum.12); 
(E) Ushirika (Mdo.2:42-46)
 
12. Uponyaji wa Mungu: 
Uponyaji wa Mungu ni sehemu muhimu ya Injili. Kufunguliwa kutoka magonjwa ni kitu kilichoko katika malipizi na ni haki ya  kila anayeamini (Isa. 53:4; 5; Mt.:8:16; 17; Yak. 5:14-16).
 
13. Tumaini lenye Baraka: 
Ufunuo wa wale ambao wamelala katika Kristo na kunyakuliwa kwao pamoja na wale walio hai waliosalia mpaka wakati wa kuja kwake Bwana ndilo tumaini lenye baraka na lililo kuu la Kanisa (1Thes.4:16,17; Rum. 8:23;  Tito 2:13; 1Kor.15:51,52.
 
14: Utawala wa Kristo wa miaka Elfu: 
Kuja kwa mara ya pili kwa Kristo ni pamoja na kunyakuliwa kwa Watakatifu ambalo ni tumaini lenye baraka, kukifuatiwa na kurudi kwa wazi kwa Kristo pamoja na Watakatifu wake kwa ajili ya kutawala hapa Ulimwenguni kwa muda wa miaka elfu moja (Zek. 14:5; Mt. 24:27;30; Ufu.1:7; 19;11-14; 20:1-6).
Utawala huu wa miaka elfu moja utaleta wokovu kwa Israeli kama taifa (Eze. 37:21,22; Zef.3: 19,Zab. 72:3-8; Mika 4:3,4).
 
15. Hukumu ya Mwisho: 
Kutakuwepo na hukumu ya mwisho ambayo humo wafu waovu watafufuliwa na kuhukumiwa sawa sawa na matendo yao. Yeyote, ambaye  hatakutwa ameandikwa katika Kitabu cha Uzima, pamoja na Shetani na malaika  zake, mnyama na nabii wa uongo, watatupwa katika adhabu ya milele katika ziwa liwakalo moto na kibiriti, ambayo ni mauti ya pili
(Mt. 25:46; Mk.9:43-48; Ufu. 19:20; 20:11-15; 21:8).
 
16. Mbingu Mpya na Nchi Mpya: 
Sisi, kulingana na ahadi yake tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya ambamo haki yakaa ndani yake (2Pet.3:13; Ufu.21:22).