USHUHUDA WA ASKOFU LAZARO : SEHEMU YA PILI

USHUHUDA WA ASKOFU LAZARO 
SEHEMU YA PILI
 
KICHWA: NATOKEWA NA SHETANI NA KUOKOLEWA NA YESU
Katika siku za ujana wangu, mimi sikuamini shetani ni kitu cha kweli, wala katika kanisa langu hakukuwepo na fundisho lolote kuhusu shetani , na pia, tulipokuwa shuleni hatukupata elimu yoyote au tamko lolote lisemalo kuwa shetani yupo. Katika kijiji nilichozaliwa kulikuwa na dini mbili tu, Dini ya kiislamu na dini ya Kikristo (Dhehebu la Kilutheri).  Mimi nilikuwa mkristo ingawa sikupenda mambo ya dini sana kama wazazi wangu walivyopenda. Tena nilipuuzia sana elimu juu ya mashetani. Waislamu katika Kijiji chetu waliamini sana nguvu za mashetani na uchawi lakini mimi sikuyasadiki hayo kabisa wala sikuyaogopa.
 
Ilikuwa siku moja saa nne usiku, nikiwa kitandani nikivuta sigara, kwa ghafla alitokea mtu mfano wa mwarabu, akiwa na taa kubwa iliyowaka chumbani kote. Macho yake yalikuwa kama nyoka, aliponiangalia niliona hali ya uadui machoni pake. Hungehitaji kufahamu kama ni mtu mbaya au mwema, kwani macho yake yalidhihirisha wazi kuwa ni adui, tena muuaji. Alisimama na taa yake kunikabili. Nilianza kujiokoa naye kwa kutupa mikono na miguu ili asinisogelee. Mara baada ya jitihada zote hizo ambazo hazikumuogopesha, niliona ametokea mtu mwingine upande wangu, na yule mtu aliyeshika taa alipomwona yule mtu aliyekuwa nami  aliogopa kama vile mbwa aliyekemewa na bwana wake, Aligeuka akakimbia na kutoweka kabisa. Yule mtu alikuwa upande wangu alipoona yule adui amekimbia, naye aliondoka na kutoweka. Mambo hayo sikuyaona kwenye ndoto bali niliyaona kwa macho yangu kwani sikuwa nimelala. Pamoja na mambo hayo yote mimi sikumfahamu Kristo kama Bwana na mwokozi wangu na sikuwahi kusikia mtu akihubiri neno la Wokovu.
 
 
NAUGUA TENA.
Wakati niliokuwa na umri wa miaka ishirini na mbili, nilishikwa na hali ya mfadhaiko wa kufa, Niliwaona madaktari lakini hawakuona kama kuna ugonjwa wowote ndani yangu , ila walinambia niache mawazo. Hali ile ilizidi ndani yangu ikanifanya niwe mlevi sana, Niliamua kulewa ili  kujisahaulisha hali iliyokuwa ndani yangu, lakini hata hivyo hali hiyo haikunitoka. 
Baada ya kuona sipati msaada kwa hayo yote, ndipo nilimwomba baba yangu aniazime Biblia. Nilijaribu kusoma Biblia lakini sikupata msaada wowote, mwisho nilisema kama Mungu yupo basi nitaweka kichwa changu juu ya Biblia kila nilalapo na kama Biblia ni neno lake basi atanisaidia. Nililalia biblia kwa muda wa miezi mitatu. Kila siku jioni, kabla sijapanda kitandani nilale nilimwomba Mungu aniruhusu niweke kichwa changu juu ya Biblia nikasema "Ee Mungu nisamehe kama kuna kitu nimekosea au kama nimenunua pombe au sikumlipa muuzaji pesa zake naahidi nitamrudishia kesho, lakini niruhusu tu niweke kichwa changu juu ya Biblia."
 
Siku moja nilipokuwa kitandani ili nilale kama kawaida nikaweka kichwa changu juu ya Biblia mara chumba changu kikatokewa na nuru kali sana iliyong'aa kuliko uwezo wa jua,  ndani ya nuru ile akatokea mtu akasema nami na kuniambia amekuja kunijulisha kuwa nitakufa!. Nikamwuliza, "Kwa nini nife?"  Akaniambia ni kwa sababu mimi ni mwenye dhambi. Nikamwambia mimi si mwenye dhambi kwa sababu nilibatizwa tangu nikiwa mtoto mdogo. Akanijibu kwamba ningelikuwa nimebatizwa nisingelikuwa natenda mambo mabaya. Nikamwuliza "mambo gani?" Ndipo aliponyoosha mikono yake akanionyesha matendo yangu yote mabaya niliyokuwa nimeyatenda tangu utoto wangu.
 
Akanambia "Je , Matendo haya ni yako?" Nikamwambia "Ndiyo" Kila tendo alilonionyesha lilikuwa kweli na nililikumbuka nilivyotenda. Nikamwambia, "Ninakubali mimi ni mwenye dhambi." kwa ajili ya matendo hayo utakufa, lakini nimetumwa nikujulishe kuwa kama utampokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wako utaokoka nawe hutakufa"  Ndipo nikamwambia ninakubali kumpokea Yesu, naye akanimbia nipige magoti ili aniongoze sala ya toba. Nikapiga magoti akaniongoza salam ya toba, na ya kumkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yangu.  Pale pale litatokea ziwa la maji na akaniambia njoo nikubatize, akanichukua na kunizamisha ndany ya maji, Akanibatiza kwa jina la baba na la mwana na la Roho Mtakatifu. Mimi kabla ya hapo sikuwa nimeona au kusikia kuwa kuna ubatizo wa kuzamishwa ndan ya maji mengi.
 
Asubuhi baba yangu aliniuliza "Ulikuwa unaongea nini usiku mwenyewe?"  Ndipo nilipomweleza yote yalionitokea na jinsi nilivyobatizwa ndani ya ziwa la maji. Kumbe nilipokuwa nasema na yule mtu nilikuwa  nikisikika hata kwenye chumba ndani ya ziwa la maji alinionya na kuniambia nipunguze ulevi. Hata baada ya kutubu kwenye yale maono sikupona ule ugonjwa nilokuwa nao mara baada ya yale maono niliondoka kwenda mjini arusha. Wakati nikiwa Arusha nilielezwa juu ya kikundi kidogo kilichouwa kinaimba na kuhubiri Injili . Mimi na wenzangu tuliamua kwenda hapo ili tukaangalie. Jambo lililotufanya twende ni kule kusikia kuwa kuna mama wa Kizungu ambaye alikuwa akiimba nyimbo za Mungu kwa kutumia gitaa . Siku zile gitaa ilitambulikana kama chombo cha shetani kabisa. kwa hiyo tulienda ili kuona dini ya kishetani inavyoimba. Tukaingia ndani mara yule mama akaanza kuimba na wimbo aliouimba maneno yake ni kama ifuatavyo. "Usisumbuke kwa safari, Mungu akulinda utegemee pendo lake , Mungu akulinda..."
 
Kabla mama yule hajamaliza kuimba, Nilishukiwa na nguvu zilizoingia moyoni na kuondoa ile hali ya siku zote ya kufa nikawa mzima kabisa. Kwa sababu zile nguvu zilisisimua mwili wangu wote, nilijikuta natokwa jasho jingi sana. Wenzangu niliofuatana nao walipigwa na mshangao wakajaribu kunituliza lakini sikuweza kusema nao , baada ya zile nguvu kutulia nikaamua kumwona huyo Mmisionari  na mke wake ili niwaulize ni kitu gani kilichonitokea na imekuwaje mtu aimbe kisha nipone. Ndipo waliponihubiria habari za Yesu na uweza wake wa kuokoka na kuponya , Na kwa kuwa alikuwa akinisomea Biblia nikadhani Biblia ile siyo kama ya kanisa letu huenda ni nyingine .
 
Ndipo nilipoamua kurudi nyumbani nikachukua biblia ya baba yangu kwa kuwa mimi sikuwa na biblia yangu. Nilipoona Biblia ya yule mmisionari na ileile ya baba yangu ni sawa neno kwa neno, na mstari kwa mstari nilishangaa na kujiuliza, "Mbona maneno ya wokovu na uponyaji hayahubiriwi kanisani kwetu?" Nilirudi tena Arusha kukutana na Yule Mmishionary, Ndipo nilipokubali kumpokea Yesu. Naye akaniongoza sala ya kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wangu.  Nilibatizwa ndani ya ziwa la aina  ile ile niliyoona kwenye yale maono. Niliamua kufata kila neno la Biblia lilivyokuwa linaeleza kuhusu wokovu. Kisha wakanifundisha juu ya ubatizo wa Roho Mtakaifu : Nikawa na hamu kubwa ya kupokea Roho Mtakatifu . Nilikesha kwa muda mrefu nikimsihi Mungu anibatize kwa Roho Mtakatifu. 
 
SHETANI ATAFUTA KUNIANGAMIZA TENA
Nikiwa natafuta ubatizo wa Roho Mtakatifu alinitokea mwanamke ambaye alikuwa amepanga chumba kilichokuwa karibu na chumba changu. Alinipenda sana akataka nizini naye, lakini upendo wa Kristo ulikuwa mkuu ndani yangu kiasi ambacho kishawishi chake hakikunitia shida yeyote bali niliendelea kumshuhudia neno la Mungu. Bila mimi kujua makusudi yake, alinitengenezea dawa, akaweka kwenye kahawa akanipa . Nilikunywa ile kahawa na baada ya kunywa nilianza kusikia kifua changu kikiwa kizito. 
 
Baadaye kikatokea kitu kifuani kama ndege na mtu akitoa sauti mbele yangu au akinisalimu kile kitu kilizunguka kifuani na kutoa miiba ambayo iliniumiza kwa maumivu makali sana. Wakati huo nilikuwa sijajazwa Roho Mtakatifu. Nilienda hosipitalini na daktari aliponipima alinambia kuwa sina ugonjwa kifuani bali ni mawazo tu. Niliendelea kuumwa na nikazidiwa sana. Yule mwanamke alipoona nakaribia kufa alinijia akiwa amejaa chuki na akaniambia kuwa haya yote yamenipata kwa sababu nilikataa kuzini naye. Wale wenzangu waliokuwa wameokoka walinieleza juu ya uponyaji wa Yesu na kunisomea maandiko ya 
"Marko 16:17-18 
<16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.
 17 Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;>"  
 
Wakaniuliza "je unaamini jina la Yesu?" nikawaambia ndio. Ndipo walipoweka mikoni juu yangu na kwa jina la Yesu wakamwamuru pepo ndani yangu anitoke, saa hiyo hiyo , kile kitu kikapiga kelele ndani yangu kikatoka nikawa mzima pale pale. Nikapigwa na mshangao mkubwa nikabakia nikiangalia kulikuwa na nini kwenye mikono yao na nilipoona hakukuwa na kitu chochote isipokuwa jina la YESU tu ndipo nilipoamua mimi na maisha yangu yote nitamtumikia Bwana Yesu. Yule mwanamke alipoona nimepona alikasirika sana na kuniambia ni lazima ataniua . Nilikuwa tayar nina ujasiri mkubwa wa jina la Yesu hivyo nikampuuzia na kumwambia "Hutaniweza kwani mimi nina jina la Yesu"  kuanzia wakati ule yule mama aliogopa sana, mwishowe alihama Arusha na hatimaye aliugua ugonjwa wa kuvimba mwili na akafa
 
Shetani aliazimia kuniua tena wakati huu waziwazi, lakini Mungu aliniandaa kwa wakati wangu ili adhihirishe Uweza wake kwa watu wa kizazi chetu, naye shetani hali akijua hayo alijitahidi kutaka kuniangamiza mara nyingi  ili kusudi la Mungu lisitimie lakini kama vile Neno lake lisemavyo katika Isaya 55:11 "Ndivyo litakavyokuwa neno langu litokalo katika kinywa changu halitanirudia bure bali litatimiza mapenzi yangu nalo litafaikiwa katika mambo yale niliyolituma" katika Yeremia 1:12 amesema "Ninaliangalia neno langu ili nilitimize"  kwa maana halisi ni kwamba Mungu hulilinda Neno lake, na kuhakikisha kuwa limefanikiwa na kutekeleza yale aliyolituma. Mimi nilishangazwa sana na matokeo ya mambo ambayo yalikuwa yakinipata kwani nilipokuwa nikiangalia wenzangu hawakuwa wakipatwa na jambo lolote mfano wa hayo.