USHUHUDA WA ASKOFU LAZARO : NAJAZWA ROHO MTAKATIFU

Nilianza kuutafuta uso wa Bwana, ili nipate ahadi ya Roho wake; nakumbuka nilikesha mbele zake kwa maombi kwa muda kama wa miezi mitatu. Siku moja tulikuwa kwenye Conference huko puge Tabora, na nguvu za Mungu zilikuwepo kwa wingi sana. Yule mtu aliyekuwa akihubiri alipomaliza alisema "wote tuseme moto" na watu wote tukasema moto. Mara zikanishukia nguvu nyingi nikajikuta nanena maneno nisiyoyafahamu. Niliendelea kunena kwa lugha kwa masaa mengi , moyo wangu ulifurika nguvu za Mungu na hapo hapo nikaanza kupokea moyo wa kwenda nyumbani kwetu Moshi nikawaeleze mambo ambayo Mungu amenitendea.
 
Tuliporudi Arusha kutoka Puge Tabora niliendelea kukesha na kuomba. Siku moja Mmisionari  tuliyekuwa naye ambaye aliitwa Claeson aliniita akaniambia "Mungu amesema nenda nyumbani kwenu" Mimi sikujua maana yake ni nini ila moyoni  mwangu nilishataka sana kwenda nyumbani niwaeleze yale yaliyonitokea. Mara nilipofika, nilienda kanisani kwetu nikamwomba Mchungaji aniruhusu niwaambie mambo ambayo Mungu amenitendea . Akaniuliza ni mambo gani nikamweleza jinsi nilivyookoka na jinsi Mungu alivyoniponya kwa jina la Yesu na jinsi nilivyojazwa Roho Mtakatifu kama mitume.
 
Mchungaji akaniambia "Siwezi kukuruhusu kwa kuwa wewe unataka kuleta dini mpya hapa" Nikamwambia sio kweli ila tu nataka kushuhudia Bwana alivyonitendea . Kwakwel mimi sikuwa na haja ya kuhubiri ila tu  hamu yangu kuwaeleza yale Bwana aliyonitendea. Nilipoona Mchungaji amekataa niliwafuata vijana nikawaeleza jinsi nilivyookoka, nilivyoponywa na kujazwa Roho. 
 
Vijana wakashangaa sana wakaniuliza "je hata sisi tunaweza kujazwa Roho vile vile kama wewe? " Nikawaambia "ndio" wakaniuliza "tufanyeje ili tupate huo ujazo?" Nikawaambia ni kwa njia ya kuomba tu. Wakaniambia "Tuko tayari tuongoze jinsi ya kuomba" Mimi nikaanza kuogopa nikifikiri kama tukiombea kanisani na Roho Mtakatifu akashuka itatokea hali ambayo viongozi wa kanisa hawataipenda, na mimi nitasumbuliwa na sikutaka niwakosee viongozi wa kanisa langu.
 
Kwa hiyo nikawaambia kama mnataka kujazwa Roho, twendeni porini tukaombee huko. Huku nikijua kama Roho akishuka huko hakuna mtu atakayetusikia. Vijana kwa kuwa walitamani sana kujazwa Roho walikubali kwenda porini bila kujali, kwa kuwa hamu yao ilikuwa ni kujazwa Roho tu