USHUHUDA WA ASKOFU EMMANUEL LAZARO. SEHEMU YA KWANZA

USHUHUDA WA ASKOFU LAZARO 
SEHMU YA KWANZA.
 
KICHWA: BWANA YESU ALINITOKEA
Nilizaliwa katika kijiji cha Modio, wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro Tanzania. Nilisoma elimu ya msingi katika shule ya msama, na baadaye nilienda Mombasa kwa mafunzo ya miaka miwili. Baba  yangu anaitwa kunandumi na mama yangu anaitwa Firayandiani . Wazazi wangu walipenda sana mambo ya dini inagawaje wakati huo neno la wokovu lilikuwa halijahubiriwa kwa hiyo hawakujua wokovu.
 
Katika siku za utoto wangu, neno la uponyaji kwa jina la Yesu halikuhubiriwa kabisa, wala hatukusikia kuwa Yesu anaweza kumponya mtu mgonjwa kwa jina lake. Nilipokuwa na umri kama wa miaka saba niliugua, hali yangu ilizidi kuwa mbaya ikabidi nilazwe kwenye zahanati ya kanisa la Kilutheri Masama. Hata hivyo hali yangu iliendelea kuwa mbaya na Daktari akataka nirudishwe nyumbani. Mwili wangu ulidhoofika sana, na kutoa harufu mbaya. Chumba nilimokuwa nikilala kilinuka harufu hiyo, na kwa ajili ya udhaifu pia sikuweza kula kabisa.
 
Nilipokuwa nikiongea , niliisikia sauti yangu nyuma ya kichwa changu. Siku moja asubui, kama saa nne niliskia baridi sana mwilini mwangu: nikamwomba mama anitoe nje ili nipate joto la jua. nikiwa nje mama aliniangalia kaanza kulia nilipomwona mama analia nilimuuliza "Unalia nini?" Akaniambia "Nalia kwa sababu nimefanya kila niwezalo ili upone lakini huponi" kwa ghafla nikatokewa na maneno haya yafuatayo   "SITAKUFA YESU NI UWEZA" nikamwambia mama.
 
Wakati maneno hayo yalipokuwa yakinitoka, yalibadilika kuwa moyo ndani ya kinywa changu, ikawa kama kunga donge la moto kinywani. Nikiwa nashangaa yanayonitokea ule moto ulishuka tumboni nikaanza kusikia joto kali katika mwili wote. Nilitokwa na jasho mwili wote na hapo hapo nikajikuta mimi ni mzima kabisa. Nikiwa sielewi ni nini kimetokea nilijiskia hamu ya kula, nikamwomba mama anipe chakula. mama hakuamini kuwa naweza kula, akaniuliza , "wewe waweza kula?" Nikamjibu "ndiyo". Akanitengenezea chakula nikala na tangu wakati ule sikuwa mgonjwa tena  "JINA LA BWANA LITUKUZWE"
 
Ingawa jambo hilo lilitokea mbele ya mama yangu sikuweza kumweleza ile hali iliyonitokea , bali ilinikaa moyoni mwangu bila kumweleza ile hali iliyonitokea , bali ilinikaa moyoni mwangu bila kumweleza mtu , Tangu zamani Mungu amekuwa akidhihirisha mambo yake yajayo na ndiyo awafunguaye vinywa wanadamu kwa wakati ulioamriwa ili wayanene. wakati nilipokuwa kwenye masomo yangu huko Mombasa niliugua tena. Hali yangu ikawa mbaya sana hata nikashindwa kula , Nilibebwa nikapelekwa katika hospitali ya madaraka Mombasa, na mjomba wagu Wilson Kimaro. 
Nilipofika hospitalini nilikaa nikimngojea Daktari aje, Wakati nipo nje ya hospitali  Mwili wangu ulionyesha hali ambayo nilihisi kama ninakufa. Mawazo yangu yakafikwa na hali ya kumwomba Mungu ingawaje sikuwa mtu mwenye hali ya kuomba wala sikuwamtu wa kutaka mambo ya Mungu kwa wakati huo. Ninakumbuka wakati huo, hofu ya kifo ilinitisha ndipo nilimwambia Mungu maneno haya "KAMA UKINIPONYA NITAKUTUMIKIA" sielewi nilipata wapi fikra hizo. Mara baada ya kusema hivyo , nilizimia nilipochukuliwa kupelewa ndani ya hospitali kulazwa sikuwa na fahamu kabisa. Kufuatana na taarifa nilizozipata baada ya fahamu zangu kunirudia daktari alisema hakuna uwezekano wa matibabu, kwa kuwa nisingeweza kupona. 
 
Nilizimia tena kwa siku tatu na daktari alikuwa anaangalia mapigo ya moyo tu. Hii ikiwa na maana alikuwa akipima kuona kama nipo hai au nimekwisha kufa. Wakati wote nilipikuwa nimezimia, niliona malaika wa Bwana akija na kunipakata , akinionyesha maua mazuri ya ajabu. Malaika huyo alikuwa akinitokea hasa wakati ambao natokewa na hali ya kutoweka kabisa (Yaani kufa). Aliendelea kunitokea hivyo mpaka niporudiwa na fahamu zangu nikajikuta nimepona. 
 
Niliwauliza wale wangonjwa waliolazwa chumba kile pamoja nami "Yuko wapi yule mtu anayeniletea maua?" wote walishangaa kuskia nimerudiwa na fahamu zangu, wakanieleza kuwa daktari alikuwa anaongea saa yangu ya kukata roho, na kwamba sikupewa dawa yoyote wala sindano tangu nilipolazwa hapo. Wala hakuna mtu yeyote aliyekuja kuniletea maua. "MUNGU NA ATUKUZWE KWA REHEMA ZAKE KWA WANADAMU"
Hata hivyo baada ya kupona sikuwa na mawazo tena kwamba nilimwahidi Mungu kuwa kama angeniponya ningemtumikia . Niliendelea kuwa mwovu kama kawaida.
 
Itaendelea sehemu ya pili........