KWA NINI WATOTO WAFIKIWE?

Utangulizi
"Huyu mtoto atakapokuwa mkubwa atakuwa kama baba yake tu bure kabisa!" Hayo maneno alikuwa anayasikia Hugo tangu akiwa mvulana mdogo. Baba yake hakuwa mfano mzuri kwakwe. Alikuwa anatumia fedha yake yote katika vilabu vya  pombe. Hugo alipotimiza miaka 14,  alipata kazi ili kusaidia gharama za maisha nyumbani. Lakini kama baba yake pia, alipoteza fedha zake katika ulevi.Mambo hayo hayakumfurahisha baba yake,  lakini angefanya nini? Alijua vitisho visingemfanya mtoto wake aache pombe.
 
Siku moja, mtu fulani alileta vijitabu vidogo shuleni kwa akina Hugo. Akakimbia haraka kujipanga mstari. Hakujua wala hakujali vile vijitabu vilikuwa vinahusu nini. Yeye alichotaka ni kitabu chake binafsi cha kusoma. Akafanikiwa kupata kitabu kimojawapo.Alipofika tu nyumbani, alisoma kile kitabu tangu mwanzo hadi mwisho.  Ilikuwa Agano Jipya. Hugo hakujua Ukristo ni kitu gani wala hakuelewa kwa nini alijisikia kuvutwa na kuendelea kusoma. Ila aliposoma nguvu za Neno la Mungu ziligusa moyo wake. Akiwa amehamasishwa kwa ujumbe wa Biblia, Hugo alikwenda kwenye kanisa la Assemblies of God na kumpokea Yesu kama mwokozi wake. siku hiyo maisha yake yalibadilika. Hakuendelea kuwa mlevi wa kupindukia kama watu walivyotazamia. Badala yake, alikuja kuwa mhubiri . Mtu fulani alimfikia Hugo akiwa kijana, na matokeo yake ni kwamba yeye anawafikia maelfu wengine.
 
shauku ya Hugo ni kuwahudumia watoto katika nchi nyingi. Yeye ni mwanachama wa timu ya kimataifa ya Latin America ChildCare (LACC). Anasafiri toka taifa hadi lingine akisaidia mashule yenye kufadhiliwa na shirika la LACC. Hugo huwasaidia watumishi wao na kuwashirikisha watoto upendo wa Mungu . Yeye pia ni mchungaji wa kanisa kubwa , na ni mchungaji wa shule zote zinazosaidiwa na LACC katika nchi ya Costa Rica, Marekani ya kusini. Pamoja na hayo ni mkurugenzi makao ya watoto walioachwa na wazazi wao au waliotendewa mabaya. Hugo Solis ni mtu mwenye tabasamu kubwa . Lakini analia sana kwa ajili ya hali za kusikitisha za watoto duniani kote. Anapokumbuka mahitaji yake ya kiroho alipokuwa mtoto humhamisha kueneza upendo wa Mungu kwa watoto.
 
Lengo la nakala hii, ni kuwasaidia wachungaji, watumishi, walezi na wale wote wenye moyo wa kusaidia watoto. je nini mahitaji ya watoto? Mchungaji anawezaje kuwahudumia watoto? Mchungaji anaweza kufanya nini ili kuliwezesha kanisa kwa ajili ya huduma kwa watoto? Tunatazama nini tunapochagua mtaala wa ajili ya watoto? kwa nini tuwahudumie watoto? Je biblia inasemaje kuhusu huduma ya watoto.
 
A. Huduma kwa watoto ni amri ya Mungu
1.  VITABU VYA MUSA VINATUAMURU TUWAFUNDISHE WATOTO.
 Kuwahudumia watoto ukweli, kuwafundisha kumpenda , Kumheshimu na kumtii Bwana, ni amri ya Mungu katika kitabu cha kutoka , Bwana alimwambia Musa awaagize watu waishike Paska Musa akawaambia waisraeli kwamba watoto wao wangewauliza sababu ya hiyo sikukuu (Kutoka 12:26). Ndipo watu walipotakiwa kuwasimulia watoto wao kuhusu ulizi wa Mungu kwa familia zao wakati walipokuwa watumwa huko misri. Tunapaswa kuwaambia watoto wetu yale ambayo Mungu ametutendea hata sisi. Tunapaswa kuwafundisha kwamba Mungu ni mwaminifu. 
 
Baada ya kumpa Musa zile Amri kumi, Mungu alisema hivi.
"Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako. Nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako na utembeapo njiani na ulalapo na uondokapo (Kumbukumgu 6:6-7)" Mpango wa Mungu si kuwafundisha watoto kwa masaa machache tu kila wiki kanisani!. Darasa la kwanza  la mtoto ni nyumbani. Wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto kuhusu Mungu kila siku, wakiwa wanacheza, wakiwa wanafanya shughuli, wakiwa wanakwenda dukani au sokoni. wakati wa kulala. Wazazi wenye busara hutafuta Fursa za kufundisha nyakati zinazowaruhusu wao kufanyia kazi kweli za maandiko katika maisha ya mtoto. Aina hiyo ya kujifunza huwasaidia watoto kupokea maarifa ya Kibiblia na kuyatumia katika maisha yao kila siku. Wazazi hutoa mfano wa jinsi ya kumpenda na kumtegemea Mungu.  Basi wazazi hutii, kumbukumbu la Torati 6:6-7 kila siku. 
 
Mvulana mdogo aitwaye Yohana alikuwa na miaka 7. Asubuhi moja wakati mama yake akiwa anasafisha vyombo alimwuliza swali la kushangaza sana, "Je ninahitaji kumwomba Martin aingie moyoni  mwangu?" akanyamaza kidogo na kuwaza, mbona kauliza swali hilo?  ndipo akatambua kwamba wakati wa igizo la pasaka, mtu mmoja aitwaye martin alimwakilisha Yesu . Yohana alimwona na kumjua Martin lakini hakuwahi kumwona Yesu , Nyumbani na kanisani aliambiwa umuhimu wa kumwomba yesu aingie moyoni mwake. Basi yohana alitaka kujua kama amwommbe Martin ambaye alikuwa anamwona aingie moyoni mwake. Mama yake Yohana akatambua kwamba hiyo ni nafasi ya kufundisha . Hakusubiri mpaka Jumapili kanisani au mpaka  wakati wa maombi ya familia jioni. Aliacha alichokuwa anafanya na 
kumweleza Yohana habari za yesu. Akaeleza maana ya kumwomba aingie moyoni mwake . Asubuhi hiyo, pale nyumbani , 
Yohana alizaliwa katika ufalme wa Mungu baada ya mama yake kusema naye na kumwombea . 
 
Kwa nini wazazi walipewa amri ya kuwafundisha watoto wao? kwa sababu watoto hupokea mafundisho ya Kikristo kwa ubora zaidi toka kwa wale wanaowapenda zaidi yaani wazazi wao. Upendo wa  wazazi hufungua mioyo ya watoto kwa ajili ya Mungu. Wachungaji wenye hekima huwaongoza wazazi kuwafundisha watoto wao kuhusu Mungu wakiwa nyumbani. Kanisa huwasaidia wazazi kwa kuongezea mafundisho ya Biblia yanayotolewa kwa watoto nyumbani . Wakati mwingine wazazi hawafundishi watoto wao habari za Mungu . Huduma ya kanisa kwa watoto kama hao ni ya muhimu sana.
 
2. VITABU VYA HEKIMA PIA VINATOA USHAURI KUHUSU KULEA WATOTO. 
Mti unapokuwa mdogo unaweza kuukunja kuelekea upande wowote unaotaka. Lakini baada ya miaka kadhaa ni vigumu sana kubadilisha jinsi mti unavyokua. Katika Mithali 22:6 , Suleimani anasema hivi: "Mlee mtoto katika njia ipasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee" wafundishe watoto wadogo kumpenda Mungu na kumtii, na kwa kawaida watakuwa waamini wenye nguvu. 
Mhubiri 12:1 inamwambia kijana mkumbuke Mungu "kabla siku mbaya hazijaja" kuwafundisha watoto kuhusu Mungu kukabiliana na majaribu yanayokuja kwa vijana na watu wazima.
 
3. KATIKA AGANO JIPYA, YESU ANASEMA WATOTO WAELEZWE HABARI NJEMA. WAFANYWE KUWA 
WANAFUNZI NA WAHUDUMIWE.
Maneno ya mwisho ya Yesu kwa wanafunzi wake yalikuwa haya "Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri injili kwa kila kiumbe" (Marko 16:15). Mungu aliwaumba watoto, naye anawaona kuwa wa maana  sana. Wanangojea kusikia habari njema kwamba Yesu anawapenda. Watu wote wana haki ya kusikia Injili kwa kiwango wanachoelewa. Kuhubiri kunaweza kusiwe njia bora ya kuwaeleza watoto. Lakini wanaelewa Injili vizuri sana kupitia nyimbo, hadithi, maigizo, na mifano ya Wakristo. Tunapowafundisha watoto habari za yesu, tunatii Agizo Kuu la Marko 16:15 katika Injili ya Mathayo , Yesu anakaza kwamba tunapaswa kufanya wanafunzi katika mataifa yote (Mathayo 28:19).
 
Katika mataifa mengi ya duniani, watoto ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu walioko. Ni lazima watoto wafanywe wanafunzi, sawa na watu wazima. Ili kuwafanya watoto kuwa wanafunzi, lazima tuwafikie na kuwafundisha , tuwasaidie kukua na kukomaa kama Wakristo.
Yesu aliamuru "Waacheni watoto wadogo waje kwangu" (Mathayo 19:14). Katika mantiki hii, Bwana alikuwa anawahudumia watu wazima. Wazazi wakaleta watoto wao kwa  Yesu na kuomba awabariki . Lakini wanafunzi waliwaambia wazazi waache kumsumbua Yesu kwa kuleta watoto . Yesu akawaagiza wanafunzi kwamba "Waacheni watoto wadogo waje" si kwamba ni wazazi tu wanaotaka kuleta watoto wao kwa Yesu. Hata watoto wenyewe huvutwa kwa Yesu. Wanapenda kuwa katika uwepo wake. Yesu alisema tusiwazuie kumwendea . Baada ya ufufuo Yesu alimwagiza Petro hivi. "Lisha wanakondoo wangu" (Yohana 21:16) . Wanakondoo wa Yesu wanahitaji chakula cha kiroho ili wakue kama tunampenda Kristo, hatutawapuuza wanakondoo wake, ambao ni watoto.
(Itaendelea.....)