KONGAMANO LA UINJILISTI DODOMA 2017

Pichani ni Makamu Askofu Mkuu wa TAG Dk.Magnus Mhiche (katikati), akiwasili kwenye ukumbi wa kongamano hilo mjini Dodoma.  Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uinjilisti, Rev.Spear Mwaipopo (kushoto), Askofu wa TAG Jimbo la Dodoma Kati Rev.Stiven  Mahinyila (kulia), wengine ni baadhi ya watu aliyoambatana nao.

 

Moja ya jambo kubwa linalotakiwa kufanyika ili kuhakikisha Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), linafikia malengo yake ya miaka kumi ya mavuno, ni kuhakikisha Injili inahubiriwa kila kona kwa nguvu zote. Kwa kutambua hilo kanisa kupitia Idara ya Uinjilisti chini ya Mkurugenzi wake Rev.Spear Mwaipopo na kamati yake, limeandaa kongamano la Wainjilisti wa TAG, ili kuwanoa na  kuchochea gia waamke upya kumhubiri Yesu Kristo kwa kila kiumbe.

Kongamano hilo la aina yake kwa mwaka huu wa 2017, ambalo upekee wake ni kutokana na mwitikio mkubwa
wa wajumbe kutoka kila kona ya Taifala Tanzania na waliojaa hamu ya kumsikiliza Mungu.
 
Mgeni rasmi wa kongamano hilo lililofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM), ilikuwa awe Askofu Mkuu wa TAG, Dk.Barnabas Mtokambali, lakini akawakilishwa na Makamu wake Askofu Dk.Magnus Mhiche. Mbali na kutokufika Dk.Mtokambali alimwagiza makamu wake afikishe salamu zake kwa wajumbe wote wa kongamano hilo.
 
UFUNGUZI
Makamu Askofu Mkuu ndiye aliyefungua kongamano hilo na wakati wa ufunguzi huo akatoa Neno la Mungu, akiwa na ujumbe usemao
WEWE NI SILAHA ZA BWANA Yeremia 51:20-23. Katika mahubiri yake aliwataka wainjilisti wote na wajumbe wa mkutano huo kutambua kuwa wao ndio Bwana anawategemea kuhakikisha kuwa jamii inabadilika na kumrudia yeye. Aliwahimiza wawe na mzigo mkubwa juu ya Taifa la Tanzania,
kwamba wahubiri Injili yenye kuleta mageuzi makubwa watu waache uovu wamgeukie Mungu. Aliwatoa wasiwasi wa kutojua lugha za kigeni bali wamuishie Mungu na kuifanya kazi yake kwa bidii kwani ndilo jambo waliloitiwa. Alikemea wainjilisti wenye majivuno na kwamba waache tabia hiyo kwani karama waliyonayo ni Bwana amewapa bure, bila gharama yoyote. Dk.Mhiche katika mafundisho yake, akawataka watumishi hao wa Mungu kutambua kuwa matukio ya kutisha yanayotokea Tanzania yatakomeshwa na silaha za Bwana. Aliwataka kufanya kazi katika mazingira ya aina yoyote na kwamba wasichague mahali pa kwenda kufanya huduma.
 

 

Pichani ni Mwinjilisti wa Kimataifa Rev.Johannes Amrtizer, akihubiri wakati wa kongamano la Uinjilisti mjini Dodoma, kushoto ni mtafsiri wake Rev.Huruma Nkone.

 

Miongoni mwa wanenaji wa kongamo hilo alikuwa mtumishi wa Mungu Mwinjilisti wa Kimataifa Johannes Amrtizer, kutoka nchini Sweden. 
Akifundisha wakati wa kongamano hilo aliwataka wajumbe wa mkutano huo kutambua kuwa kazi kubwa waliyoitiwa na Mungu ni kuhubiri Injili. 
Akiwa na somo alilolipa kichwa cha HUDUMA YA MWINJILISTI, Mwalimu huyo alitaka wajumbe wa kongamano hilo kutambua kuwa wao wanambeba Yesu aliyepakwa mafuta. 
Aliwataka wainjilisti wasijidharau na kujishusha na kwamba watambue kuwa walie nae ni mkubwa kuliko wanavyofikiri. 
Aliwataka watambue kuwa wamepakwa mafuta na Mungu mwenyewe hivyo wafanye kazi kwa kujiamini na kwamba wasiangalie nyuma. 
 
Pia katika mafundisho yake alihimiza juu ya kujali afya zao, Yeremia 38:7, alisema ili mwinjilisti aweze kuhubiri Injili yenye afya lazima yeye mwenyewe awe na afya. 
Mwinjilisti huyo aliwakumbusha wajumbe wa mkutano huo kutambua kuwa ili kazi yao ipate kibali mbele za Mungu lazima wazingatie kuwa na neema ya Mungu. 
Alisema Neema inamvua nguvu shetani, Neema huwafundisha kusema hapana kwa dhambi Tito 2:11-12. 
Alisema Neema hufanya kazi kwa nguvu kuliko mtu mwenyewe. 
 
Pia alisema Neema hutolewa kwa watu walio wanyenyekevu mbele za Mungu. 
Hivyo Mwinjilisti huyo akawataka wa jumbe hao kuhakikisha kuwa wananeema ya Mungu katika maisha yao ili kazi ya Mungu iimarike kila iitwapo leo.